7 Aprili 2025 - 23:08
Source: Parstoday
Watoto laki 6 wa Kipalestina Gaza katika hatari ya kupata ulemavu

Wizara ya Afya katika Ukanda wa Gaza imesema hatua ya Israel ya kuzuia kampeni ya chanjo ya ugonjwa wa kupooza wa polio inawaweka malaki ya watoto wa Kipalestina katika hatari ya kupata ulemavu wa kudumu.

Katika taarifa yake, wizara hiyo imesema watoto 602,000 huko Gaza wako katika hatari ya kupooza viungo vya mwili, kupata ulemavu wa kudumu na magonjwa mengine sugu iwapo hawatapokea chanjo za polio zinazohitajika sana.

"Kuzuia kuingia kwa chanjo kunamaanisha kuporomoka kwa juhudi zilizofanywa katika kipindi cha miezi saba iliyopita, hii inamaanisha kuwa, mzigo wa athari kubwa na mbaya zitaongezeka kwenye mfumo wa afya uliodorora, " imeonya.

Kadhalika Wizara ya Afya katika Ukanda wa Gaza imetoa indhari kuwa, kuzuiwa kampeni ya chanjo ya polio kutazidisha athari hasi za kijamii na kiuchumi katika eneo hilo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu.

Wakati huo huo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF limesema, watoto zaidi ya milioni moja wa Ukanda Gaza wanakabiliwa na upungufu mkubwa wa misaada ya kibinadamu wakati huu ambapo utawala ghasibu wa Israel umezuia kikamilifu misaada yote ya kibinadamu ya kuokoa maisha kuingizwa katika eneo hilo.

Watoto laki 6 wa Kipalestina Gaza katika hatari ya kupata ulemavu

Aidha UNICEF imeonya kuwa, watu zaidi ya milioni moja, wakiwemo watoto 400,000, wapo katika hatari kubwa ya kuandamwa na miripuko ya maradhi kutokana na matumizi ya maji yasiyo salama katika Ukanda wa Gaza.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Palestina UNRWA, asilimia 51 ya wakazi wa Ukanda wa Gaza ni watoto ambao ndio asilimia kubwa zaidi ya wahanga wa hujuma na mashambulizi ya Israel.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha